Na Beatrice Lyimo
MAELEZO
PATO
la Taifa limeendelea kukua kwa asilimia 7.9 katika kipindi cha mwezi
Aprili hadi Juni 2016 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 5.8 katika
kipindi kama hicho mwaka 2015.
Takwimu hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu hali ya pato la Taifa kwa robo ya pili kuanzia Aprili hadi Juni mwaka 2016.
Dkt Chuwa alisema kuwa ukuaji wa pato la Taifa umetokana na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, misitu na uvuvi ambapo shughuli hizo zilikuwa kwa asilimia 3.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
Kwa
upande wa shughuli za uchumi za viwanda na ujenzi, Dkt. Chuwa alisema
kumekuwa na ongezeko la asilimia 20.5 katika kipindi hicho ukilinganisha
na ukuaji wa asilimia 11.2 mwaka 2015 katika shughuli za uchimbaji
madini, mawe na kokoto.
Aidha
katika shughuli za uzalishaji bidhaa na viwanda kumeongeza kwa asilimia
9.1 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2016 ukilinganisha na kasi
ya asilimia 5.2 ya mwaka 2015.
Katika
shughuli za uchukuzi na uhifadhi, Dkt Chuwa alisema kuwa shughuli hizo
zimekuwa kwa kiwango cha asilimia 30.6 zimetokana na usafirishaji wa
abiria kwa njia ya reli na barabara ikiwa ni pamoja na usafiri wa UDART.
Hata
hivyo katika shughuli za fedha na bima ziliongezeka kwa kasi ya
asilimia 12.5 ikilinganishwa na asilimia 10.0 iliyopatikana katika
kipindi kama hicho mwaka 2015.
Wakati
huo huo huduma za elimu zilikuwa kwa kasi ya asilimia 8.0 katika robo
hiyo ya mwaka ikilinganishwa na aslimia 7.4 ya kipindi kama hicho kwa
mwaka 2015 ambapo ukuaji wa shughuli hii imetokana na ongezeko la
wanafunzi waliodahiliwa mwaka 2016.
No comments:
Post a Comment