Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
07/09/2016
Serikali
inaendelea kutangaza Kimondo kilichopo Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya
ikiwa ni kivutio muhimu na adimu nchini na duniani kwa ujumla.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Kamani
leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Vwawa Mhe. Japhet Hasungu lililohusu mpango wa Serikali katika kuhamasisha watalii wa ndani na nje kuja kuangalia Kimondo hicho.
Naibu
Waziri huyo amesema kuwa Serikali imekuwa inaendelea kuhamasisha kwa
kukitangaza Kimondo hicho kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo vipindi
vya runinga na nakala za machapisho mbalimbali.
“Uhamasishaji
umefanyika kwa kutumia njia mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwa ni
pamoja na vipindi vya runinga vya ZAMADAMU na Utalii wa ndani na kutumia
machapisho ya Tanzania ya “The land of great Heritage Sites” na
“Tanzania Cultural Heritage Resources” ambapo nakala zake husambazwa
katika maonesho mbalimbali na Balozi zetu pamoja na jarida la “Ifahamu
Idara ya mambo ya kale”” na jarida la Maliasili,” alifafanua Naibu
Waziri huyo.
Aidha,
Mhandisi Kamani aliongeza kuwa juhudi hizo limepelekea ongezeko la
idadi ya watalii na mapato ambapo kati ya mwaka 2012/2013 na 2014/2015
watalii waliongezeka kutoka 990 hadi 1,681 pamoja na mapato kuongezeka
kutoka shilingi 811,000 hadi 2,426,00.
Mbali
na hayo, Mhandisi Kamani alitoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi
na wadau wengine kujitokeza kuboresha mazingira na miundombinu ya eneo
la kimondo hicho ili kuweza kuzidi kuvutia watalii wengi na kuongeza
pato la taifa.
Kimondo
hicho kinaendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia katika
masuala ya utalii ambapo kinaaminiwa kuwa ni kati ya vimondo nane
vikubwa zaidi duniani kinachokadiriwa kuwa na uzito wa tani 12, urefu wa
mita 3.3, upana wa mita 1.63 na kimo cha mita 1.22.
No comments:
Post a Comment