Social Icons

Pages

Blogger templates

Featured Posts

Thursday, April 5, 2018

“FEDHA ZA UPANUZI WA VITUO VYA AFYA ZIFANYE ZAIDI YA KAZI ILIYOTARAJIWA”, RC GALLAWA


Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akizungumza na mafundi wanaojenga katika kituo cha Afya Isansa Wilaya ya Mbozi, kituo hicho cha Afya kimepokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho.
  Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akizungumza na baadhi ya watendaji na wananchi wa kijiji cha Iyula waliojitokeza katika eneo la ujenzi katika kituo cha Afya cha Iyula Wilaya ya Mbozi, kituo hicho cha Afya kimepokea shilingi milioni 400 kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho.
 
Grace Gwamagobe-Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa amesema atahakikisha anasimamia kwa ukaribu fedha zilizotolewa na serikali Mkoani hapa kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya afya ili zifanye kazi zaidi ya ile iliyopangwa awali kutokana na kuongezeka kwa nguvu za wananchi.
Gallawa ameyasema hayo mapema jana wakati wa ziara yake Wilaya ya Mbozi alipokagua maendeleo ya upanuzi wa vituo vya afya vya Isansa kilichopokea milioni 500 na kituo cha Afya cha Iyula Kilichopokea milioni 400, kwa ajili ya ujenzi wa maabara, nyumba ya daktari, chumba cha upasuaji, jengo la mama na mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti.
“Fedha hizi lazima zifanye kazi iliyopangwa vizuri na pia tuongeze kazi nyingine ya ziada kutokana na kuwa tumepata nguvu ya wananchi lakini pia mafundi wetu hawa tunaowatumia ni wazawa na wenyeji wa maeneo ya kwetu kwahiyo gharama zao zitatupa unafuu ambao tunatakiwa kuutumia kuongeza kazi nyingine”, amesema Gallawa.
Ameongeza kuwa licha ya upanuzi wa vituo vya afya kuchelewa kuanza bado ana Imani kuwa wataweza kumaliza ndani ya muda uliopangwa kutokana na uchapakazi wa mafundi wazawa wa maeneo hayo.
Gallawa amesema kukamilika upanuzi wa vituo hivyo vya afya kutavifanya vituo hivyo vivutie na hata mgonjwa akifika apate matumaini ya kupona na sio kukatishwa tamaa na hali mbovu ya mazingira.
“Tiba ya kwanza ya mgonjwa akifika kituo cha afya akute mazingira yanavutia na sio majengo mabovu na uchafu hivyo vitamfanya akate tamaa ya kupata matibabu sahihi, tukimaliza ujenzi wa hayo majengo tutahakikisha tunapaka rangi paa za majengo yote zifanane ili vituo vyetu vya afya vivutie”, amefafanua Gallawa.
Aidha Gallawa amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Lauteri Kanoni kuhakikisha anaweka mfumo wa maji safi katika vituo hivyo hasa mfumo wa kuvuna maji ya mvua ili vituo vikikamilika maji yawepo kwa ajili ya matumizi.
Naye Mkazi wa kijiji cha Isansa Wilaya ya Mbozi Bi Stela Mkeya ameonyeshwa kufurahishwa na upanuzi wa kituo cha Afya Isansa huku akieleza baadhi ya kero walizokuwa wakizipata awali.
“Tunaishukuru sana serikali ya Magufuli kwakweli wametusaidia, tulikuwa tunapata shida kufuata huduma za upasuaji wa akina mama wajawazito huko hospitali ya Wilaya iliyopo Vwawa lakini pia hapa kwenye kituo cha afya mzazi akijifungua hata mazingira ya kwenda kujisafisha vizuri kama vile mabafu yakiwa hayatoshi kabisa”, ameeleza Bi Mkeya.
Kwa upande wao mafundi waliokabidhiwa kazi ya upanuzi wa vituo hivyo vya Afya wameonyesha ari ya kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na haraka huku wakimuomba Mkuu wa Mkoa Chiku Gallawa awasaidie upatikanaji wa taa ili waweze kufanya kazi mchana na usiku naye Mkuu wa Mkoa amekubaliana na mapendekezo hayo.

Thursday, February 22, 2018

MHE BITEKO: "MULUGO WEWE NI NOMA...!"


 
Naibu Waziri wa wizara ya madini Mhe Doto Mashaka Biteko (Kushoto) akizungumza jambo na Mbunge wa Jimbo la Songwe Mhe Philiph Mulugo wakati wa mkutano na wachimbaji wadogo uliofanyika katika kijiji na kata ya Saza, Wilaya na Mkoa wa Songwe, Leo 22 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Baadhi ya wachimbaji wadogo wakimsikiliza Naibu Waziri wa wizara ya madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa mkutano na wachimbaji wadogo uliofanyika katika kijiji na kata ya Saza, Wilaya na Mkoa wa Songwe, Leo 22 Februari 2018.
Naibu Waziri wa wizara ya madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisisitiza jambo wakati wa mkutano na wachimbaji wadogo uliofanyika katika kijiji na kata ya Saza, Wilaya na Mkoa wa Songwe, Leo 22 Februari 2018.

Na Mathias Canal, Songwe

Naibu Waziri wa wizara ya madini Mhe Doto Mashaka Biteko amesifu juhudi za mbunge wa Jimbo la Songwe Mhe Philiph Mulugo kutokana na uwajibikaji mkubwa katika kuwasemea wananchi wa jimbo hilo hususani katika kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia sekta ya Madini.

Mhe Biteko ametoa pongezi hizo kwa mbunge huyo wakati akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji na Kata ya Saza akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Songwe.

Naibu waziri huyo alisema kuwa mbunge huyo amekuwa mstari wa mbele katika kuwatetea wananchi wake hususani katika kuchochea shughuli za maendeleo ili kuongeza ufanisi wa maendeleo endelevu ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla wake.

Pongezi hizo zinajili wakati ambapo mbunge Mulugo amefanikiwa kutatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya kikundi cha TUJIKOMBE na Kampuni ya Bafex kwenye eneo la uchimbaji dhahabu la mlima Elizabeth.

Katika kumaliza mgogoro huo kampuni ya Bafex imekubali kugharamia mradi utakaochaguliwa na kikundi hicho kama fidia ya gharama walizozitumia wachimbaji hao kuendeleza eneo hilo.

"Mheshimiwa Mulugo wewe ni hazina ya Songwe, namuomba Mungu aendelee kukutunza kwaajili ya watu hawa. Mimi nipo Bungeni muda wote wewe ajenda yako ni watu wako na unafanya hivyo bila kuchoka. Kwakweli wewe ni NOMA" Alisema Mhe. Biteko huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Sambamba na hayo pia amempongeza Mbunge huyo kwa ushirikiano mzuri baina yake na serikali ya Wilaya pamoja na Chama Cha Mapinduzi jambo ambapo linaakisi uwajibikaji wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa kilio hicho cha wananchi kimedumu kwa muda mrefu hivyo jukumu la serikali ni kutatua kero za wananchi sio kuchochea migogoro.

"NI BORA TUKAWIE LAKINI TUFIKE" MHE BITEKO


Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua kinu cha kuchakata dhahabu mara baada ya kutembelea mgodi wa uchimbaji dhahabu wa Shanta Gold Mine uliopo katika Kijiji na Kata ya Saza akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Songwe, Leo 22 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua baadhi ya mitambo ya uchenjuaji madini katika mgodi wa uchimbaji dhahabu wa Shanta Gold Mine uliopo katika Kijiji na Kata ya Saza akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Songwe, Leo 22 Februari 2018.
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua njia ya kwenda kwenye mgodi wa chini mara baada ya kutembelea mgodi wa uchimbaji dhahabu wa Shanta Gold Mine uliopo katika Kijiji na Kata ya Saza akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Songwe, Leo 22 Februari 2018.
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wafanyakazi wa mgodi wa Shanta uliopo katika Kijiji na Kata ya Saza Wilayani SongweLeo 22 Februari 2018.

Na Mathias Canal, Songwe

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amesifu utendaji unaofanywa na kampuni ya uchimbaji madini ya dhababu wa Shanta Gold Mine kwa kukubali kuendana na matakwa ya serikali kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za nchi katika sekta hiyo.

Alisema kuwa Wizara hiyo imedhamiria kuboresha sekta ya Madini ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali hiyo ambayo imechezewa na wajanja wachache katika kipindi cha muda mrefu.

Mhe Naibu Waziri huyo ametoa kauli hiyo Leo 22 Februari 2018 wakati akizungumza na wafanyakazi wa mgodi wa Shanta uliopo katika Kijiji na Kata ya Saza Wilayani Songwe.

Kampuni ya SGM haipo kwenye kundi la wawekezaji walalamikaji kuwa serikali kupitia sheria ya madini inawakimbiza wawekezaji jambo ambapo sio kweli badala yake serikali imeweka utaratibu yakinifu wa uchumi fungamanishi utakaoboresha sekta ya Madini na kuwanufaisha watanzania.

"Twendeni kwa watanzania tukawaulize wamenufaika  kwa kiasi gani na uwepo wa migodi mbalimbali ya uchimbaji nchini, jibu ni jepesi tu kuna watu wachache wamenufaika na rasilimali hiyo jambo ambapo hatutalifumbia macho tena" Alisema Mhe Biteko na kuongeza kuwa

"Serikali inahitaji wawekezaji ambao wanafuata sheria Na taratibu za nchi hata kama ni wachache wanapaswa kufahamu kuwa wanapaswa kufuata sheria kwani kufanya hivyo sio ombi bali ni lazima"

Aliongeza kuwa Wizara ya Madini itaendeleza ushirikiano kwa kiasi kikubwa na mgodi huo ili kuinua zaidi uwekezaji wao na hatimaye kuwa na uzalishaji wenye tija ambao utapelekea serikali kukusanya kodi kwa kiasi kikubwa kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla wake. 

Alisema kuwa watumishi wote katika Wizara ya Madini na wawekezaji katika sekta ya madini wanapaswa kusimamia haki katika utendaji wao huku wakiunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha nidhamu ya uwajibikaji hususani kujitenga na utoaji ama upokeaji wa rushwa.

Alisema dhamira ya serikali ya awamu ya tano ni kuwarahisishia huduma wachimbaji wadogo kupitia malezi bora ya Wizara ya madini ili kufikia hatua ya kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye kufikia uwekezaji mkubwa katika uchimbaji wa rasilimali hiyo.

Katika hatua nyingine wawekezaji hao wametakiwa kuwaamini wataalamu wa Madini wa hapa nchini pasina kuwa na Mashaka nao kwani serikali inawafahamu na wengi wao wakiwa wanafanya kazi nje ya nchi.

NAIBU WAZIRI MADINI ATUA MKOANI SONGWE KWA ZIARA YA KIKAZI


Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza mara baada ya kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Songwe kwa ajili ya ziara ya siku mbili ya kikazi katika mkoa wa Songwe, Leo 22 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisisitiza jambo mbele yaKamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya songwe, na Kamati ya  siasa ya CCM Wilaya hiyo mara baada ya kuwasili Mkoani Songwe kwa ziara ya kikazi, Leo 22 Februari 2018.
Mkuu wa wilaya ya Songwe Mhe Samwel Jeremiah akieleza changamoto za wachimbaji wadogo katika Wilaya hiyo mbele ya Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati akisoma taarifa ya Mkoa wa Songwe kwa niaba ya mkuu wa Mkoa huo Mhe Chiku Galawa, Leo 22 Februari 2018.


Na Mathias Canal, Songwe

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko leo 22 Februari 2018 ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Songwe ambapo pamoja na mambo mengine atatembelea na kukagua eneo la mgodi tarajiwa wa Bafex linalotarajiwa kuanza uchimbaji wa Madini ya dhahabu.

Maeneo mengine atakayotembelea ni pamoja na mgodi wa uchimbaji dhahabu wa Shanta Gold Mine uliopo katika kata ya Saza, Wilayani Songwe ambapo atazungumza pia na wafanyakazi wa mgodi huo.

Sambamba na hayo pia Naibu Waziri wa Madini atazungumza na wachimbaji wadogo kwenye mkutano ulioandaliwa Mara baada ya kutembelea maeneo ya uchimbaji.

Mara baada ya kuwasili katika Mkoa wa Songwe Mhe Biteko amesifu juhudi za mbunge wa Jimbo la Songwe Mhe Philiph Mulugo kutokana na uwajibikaji mkubwa katika kuwasemea wananchi wa jimbo hilo hususani katika kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia sekta ya Madini.

Alisema kuwa mbunge huyo amekuwa mstari wa mbele katika kuwatetea wananchi wake katika katika kuchochea shughuli za maendeleo ili kuongeza ufanisi wa maendeleo endelevu ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla wake.

Aidha, Mhe Biteko alimuhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Songwe kuwa Wizara ya Madini Kupitia sheria mpya ya madini kutakua na Tume ya Madini ambayo kimuundo itakua na Afisa madini wa Mkoa wa Songwe ambapo utapelekea kuwa na Ofisi hiyo ya Madini.

Mhe Biteko aliutaka uongozi wa Wilayani na Mkoa wa Songwe kuongeza zaidi ushirikiano na Chama Cha Mapinduzi kwani ndicho Chama chenye dhamana ya kuisimamia na kuikosoa serikali pindi inapoenda mrama.

Alisema kuwa baadhi ya watumishi wanapaswa kutambua kuwa wanatekeleza wajibu wa matakwa ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2015-2020 hivyo haijalishi kuwa wanaipenda ama wanaichukia wanatakiwa kutekeleza ilani pasina kuogofya.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Songwe Mhe Philiph Mulugo alisisitiza kuwa ujio wa Naibu Waziri wa Madini utakuwa chachu ya mwanzo mzuri wa maendeleo ya wananchi kupitia sekta hiyo.

Awali akisoma taarifa ya Mkoa wa Songwe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe Samwel Jeremiah ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songwe alizitaja changamoto zinazoukabili Mkoa huo katika sekta ya madini kuwa ni pamoja na kukosekana Ofisi ya Madini ya Mkoa.

Changamoto zingine ni pamoja na ukosefu wa Vifaa pamoja na elimu ndogo juu ya sheria zinazosimamia shughuli za uchimbaji Madini, pamoja na wachimbaji wengi kutokuwa waaminifu katika ulipaji wa maduhuli ya serikali yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa Madini.

Naibu Waziri wa Madini atakuwa katika ziara ya kikazi Mkoani Songwe kwa siku mbili kuanzia leo 22 Februari 2018 na kufika ukomo hapo kesho 23 Februari 2018 ambapo ataelekea mkoa wa Rukwa.

Tuesday, February 20, 2018

MHE BITEKO AWAHAKIKISHIA WANANCHI WALIOWAHI KUWA WAFANYAKAZI WA MGODI WA KIWIRA KULIPWA STAHIKI ZAO


Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wananchi waliowahi kuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira wakati akiwa ziarani Mkoani Songwe na Mbeya kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini, Leo 20 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-WazoHuru Blog
Baadhi ya wananchi waliowahi kuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko alipokuwa akizungumza jambo wakati akiwa ziarani Mkoani Songwe na Mbeya kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini, Leo 20 Februari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wananchi waliowahi kuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira wakati akiwa ziarani Mkoani Songwe na Mbeya kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini, Leo 20 Februari 2018.

Na Mathias Canal, Songwe

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amewahakikishia baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe na Wilaya ya Rungwe na Kyela Mkoani Mbeya kuwa serikali inamalizia mchakato wa uhakiki wa madeni yote ya wadai hivyo pindi itakapomaliza mchakato huo wadai wote watalipwa madeni yao.

Naibu Waziri, Mhe Biteko ametoa kauli hiyo leo 20 Februari 2018 akiwa Kijijini Kapeta, Kata ya Ikinga Wakati akizungumza na wananchi waliowahi kuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira waliosimamisha msafara wake wakati akiwa ziarani Mkoani Songwe na Mbeya kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini.

Alisema kuwa wananchi hao ndio walioiweka serikali ya awamu ya tano madarakani hivyo serikali haina haiwezi kuwasahau ama kutosimamia haki yao bali wanapaswa kuwa wavumilivu wakati serikali inajiridhisha na madeni hayo kabla ya kuanza kulipa ili kuwa na uhakika na watu wanaostahili malipo hayo.

"Watumishi lazima tukubali kwamba madeni haya tumeyarithi hayakuwa ya serikali bali yalikuwa ya muwekezaji sasa ili serikali iweze kuyalipa ni lazima ijiridhishe isije ikaingia mkenge wa kulipa watu wasiostahili kwani madeni hayo ni makubwa na yanahitaji kujiridhisha" Alisema Mhe Biteko na Kuongeza kuwa

"Sisi serikalini tunalifanyia kazi jambo lenu na tumeshafanya kazi kwa kiasi kikubwa mpaka sasa ya kuona namna ya kuwalipa na ninataka niwahakikishie kuwa kila mwenye haki anayedai lazima atalipwa lakini mtuvumilie tumepita kwenye michakato mingi ya kuibiwa fedha kwa watu kupachika madeni ya watu wasiostahili kulipwa tena wengine walishafariki"

Mhe Biteko aliongeza kuwa serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli inatambua kuwa mgodi wa Kiwira na mradi wa uchimbaji makaa ya mawe wa Kabulo ni miradi ya kimkakati katika Wizara ya Madini hivyo inatambua umuhimu wake na tayari ipo mbioni kuanzisha tena uzalishaji katika mgodi huo ambao uzalishaji wake ulisimama tangu mwaka 2009.

Alisema kuwa wananchi wamesubiri kwa muda mrefu malipo yao lakini tatizo kubwa ilikuwa ni serikali kujiridhisha na kuanisha wanufaika wa madeni hayo hivyo serikali italimaliza jambo hilo na itabaki kuwa historia.

Alisisitiza kuwa katika maeneo mengi kulikuwa na changamoto mbalimbali lakini tayari serikali imezipatia ufumbuzi changamoto hizo na wananchi wanaona utofauti.

Akijibu maswali ya wananchi hao waliotaka kufahamu ni lini mradi huo utaanza uzalishaji, Mhe Biteko alisema kuwa ili mradi uweze kuanza zipo taratibu za kisheria ambazo lazima zifuatwe ili yasijejitokeza matatizo ya kisheria baadae hivyo zitakapomalizika haraka mradi huo utaanza uzalishaji na wananchi watajipatia ajira.

DED MNASI AFANYA ZIARA YA KUKAGUA MIRADI YA UJENZI WA MADARA YA SHULE ZA MSINGI ZA WILAYA YA ILEJE

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Ileje Haji Mnasi akifanya kazi kwa vitendo alivyokuwa anafanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Izuba na shule ya msingi Ilulu na kuhakikisha wananchi wanachangia nguvu zao kuleta maendeleo kwenye vijiji vyao” alisema Mnasi
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Ileje Haji Mnasi akifanya kazi kwa vitendo alivyokuwa anafanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Izuba na shule ya msingi Ilulu
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Ileje Haji Mnasi akibadilisha mawazo na baadhi ya viongozi walikuwa kwenye eneo la ujenzi wa  madarasa katika shule ya msingi Izuba na shule ya msingi Ilulu

Na Fredy Mgunda,Ileje

HALMASHAURI ya wilaya ya Ileje mkoani songwe imetumia zaidi ya shilingi milioni mia moja themanini katika  ujenzi wa madarasa kwa kutumia fedha za EPFR ambazo hutolewa na serikali kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu kwa shule za msingi.
 
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukagua miradi hiyo,mkurugenzi wa Ileje Haji Mnasi alisema kuwa jukumu la uongozi ni kuhakikisha kuwa pesa inayotolewa na serikali inatumika kama ilivyokusudiwa na serikali kuu kwa faida ya sekta ya elimu.

“Serikali inatoa pesa nyingi sana hivyo tusipo simamia vizuri pesa hizi zitapotea kitu ambacho Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Maguli hataki kabisa kusikia kuna pesa ambayo haitumiki kama ilivyokusudiwa ndio maana nimeamua kuanza kukagua miradi yote ambayo inatekelezwa katika halmashauri yetu” alisema Mnasi 

Mnasi aliwaomba wananchi kuchangia nguvu zao kuhakikisha shughuli za ujenzi wa madarasa na vituo vya afya wanajitolea vilivyo ili kuendelea kufanya kazi sambamba na kasi ya serikali ya awamu ya tano.

“Mimi binafsi nawaomba wananchi wajitolee kufyatua tofali ,kuchota maji,kubeba mchanga na kusomba tofali ambazo zinakuwa zimenunuliwa na serikali kwa ajili ya ujenzi ambao utakuwa na faida kwao na vizazi vijavyo” alisema Mnasi

Aidha Mnasi aliwapongeza wananchi wa halmashuri ya Ileje kwa kuendelea kujitolea kufanya kazi kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya wamu ya tano ambayo imelenga kuleta maendeleo kwa wananchi wake

“Mpaka sasa kuna asilimia kubwa ambayo wananchi wamekuwa wakijitolea kufanya kazi za kimaendeleo ambazo zinawahusu japo sio kwa asilimia kubwa kutokana na idadi kubwa ya wananchi wanaoishi katika wialya hii hivyo nitoe wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kwenye maendeleo ili kuijenga ileje yetu mpya” alisema Mnasi

Mnasi alisema kuwa kipaumbele cha halmashauri kwa sasa ni kuhakikisha kuwa wanaboresha sekta ya elimu na sekta ya afya ili kukuza maendeleo ya wilaya kwa kasi kubwa.

“Ujenzi unaendelea ni wa madarasa ya shule ya msingi Izuba na shule ya msingi Ilulu na kuhakikisha wananchi wanachangia nguvu zao kuleta maendeleo kwenye vijiji vyao” alisema Mnasi

Naomba nimalizie kwa kupongeza serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Maguli kwa kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kwa kuboresha sekta za elimu,miundombinu afya na n.k