Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa
KIASI cha Sh 55,632,929 zimerejeshwa wilayani Songwe ikiwa ni sehemu
ya hasara ya fedha ambazo serikali ilipata kutokana na malipo ya
watumishi hewa katika wilaya nne za mkoa huo.
Katika uhakiki wa watumishi hewa uliofanyika Machi mwaka huu ikiwa ni
utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli wilaya nne za mkoa wa Songwe
ziliambatanishwa na zile za mkoa wa Mbeya kuhakikiwa kwa kuwa Mkuu wa
Mkoa huo mpya, Chiku Galawa alikuwa hajawasili mkoani kwake.
Kutokana na uhakiki huo, watumishi 32 kutoka halmashauri za Mbozi,
Tunduma, Momba na Ileje walibainika kuwa hewa, na walikuwa wameiingizia
serikali hasara ya jumla ya Sh 141,994,061 kwa malipo ya mishahara.
Akizungumza ofisini kwake jana, Mkuu wa Mkoa, Galawa alisema baada ya
kufika alitoa mwezi mmoja kwa maofisa utumishi kurejesha fedha hizo.
Alisema hadi juzi fedha zilizokuwa zimerejeshwa ni Sh 55,632,929 hivyo
kiasi kilichosalia kwa halmashauri hizo ni Sh 86,361,381.
Alisema kwa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi iliyosababisha hasara ya
Sh milioni 69.07 kutokana na kuwa na watumishi hewa 10 imekwisharejesha
Sh milioni 28.7, hivyo bado Sh milioni 40.3.
Momba iliyokuwa na watumishi hewa 11 ilikuwa na hasara ya Sh milioni
34.4 imerejesha Sh milioni 6.7 na bado Sh milioni 27.7 na Ileje
iliyokuwa na watumishi hewa sita ilikuwa na hasara ya Sh milioni 22.8,
imerejesha Sh milioni 20.1 bado Sh milioni 2.2 na Halmashauri ya Mji wa
Tunduma iliyokuwa na watumishi hewa watano ilisababisha hasara ya Sh
milioni 16.6 na haijarejesha kiasi chochote.
Galawa alisema hajafahamu iwapo fedha zinazorejeshwa zinatoka katika
mifuko binafsi ya maofisa utumishi, bali inapobidi itawalazimu kufanya
hivyo kwa kuwa lazima fedha za serikali zirejeshwe zote katika muda
alioagiza.
Alisema taarifa alizonazo ni kuwa zipo baadhi ya fedha zilizokutwa
kwenye akaunti za watumishi ambao ni marehemu, walioacha kazi au
kustaafu waliokuwa wakiendelea kulipwa mishahara, lakini hawakuchukua
fedha hizo benki.
Chanzo Gazeti la Habari leo
No comments:
Post a Comment