Social Icons

Pages

Blogger templates

Tuesday, July 4, 2017

UTAMADUNI WA KUFANYA KAZI NI NJIA YA KUFIKIA LENGO LA TANZANIA YA VIWANDA.



UTAMADUNI WA KUFANYA KAZI NI NJIA YA KUFIKIA LENGO LA TANZANIA YA VIWANDA.
Na Zawadi Msalla-WHUSM
Watumishi wa Mkoa wa Songwe wameshauriwa kuwa na utamduni wa kufanya kazi kwa  bidii ikiwa ni nyenzo muhimu ya kufikia malengo na azma iliyowekwa na Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa  nchi  ya Viwanda.
Hayo yamezungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Prof. Elisante Ole Gabriel wakati alipokutana na Sekretarieti ya Mkoa huo,na kuwaeleza  kuwa ni wakati muafaka kwa watumishi kupata  na kutoa elimu sahihi ya kuwafanya wananchi wapende utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii bila kulazimishwa.
” Ni vizuri watumishi wakawa na elimu ya kutosha kuhusu utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya kiutumishi ili kuweza kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kufanya kazi kwa maendeleo ya nchi yetu” alisema Prof.Gabriel
Prof. Elisante aliongeza kuwa  ni muhimu  kwa watumishi wa Umma na watanzania kwa ujumla kufanya  kazi  kwa kushirikiana  ili kutekeleza  majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya taifa .
Aidha alieleza kuwa ni budi Watanzania kufuata maadili na kuzingatia muda katika  utunzaji  wa rasilimali za nchi kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho kwa kuwa ni vigumu kutegemea mtu kutoka nje ya nchi  kutunza rasilimali za nchi yetu.
Vilevile Katibu Mkuu Prof.Elisante aliwaomba watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa  wa Songwe kuunga mkono jitihada za Rais John Pombe Magufuli za kuipeleka mbele nchi katika uchumi wa kati na kuwa Tanzania ya Viwanda.
 Mbali na hayo Prof.Elisante aliipongeza Wilaya ya Ileje kwa kuwa mfano katika utendaji uliopelekea  mafanikio makubwa kwa mkoa wa Songwe na kuzitaka Wilaya nyingine kuiga mfano huo.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa Bw.Herman Tesha aliahidi kutekeleza ushauri ulitolewa na Katibu Mkuu Prof.Elisante licha ya uchanga wa mkoa wake kwa kuwa  anaamini mwamko na ari ya watumishi waliopo kwa pamoja wanaweza kuleta maendeleo.
MWISHO


No comments:

Post a Comment