Na Benny Mwaipaja, Songwe/Mbeya
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewasimamisha kazi watumishi
wanne wa Idara ya Forodha, katika Mpaka wa Tanzania na Zambia, Mjini
Tunduma, ili kupisha uchunguzi wa kudaiwa kuhusika na upotevu wa lakiri
10 zinazotumika kufunga kwenye shehena ya mizigo inayopita mpakati hapo
kutoka nje ya nchi.
Mpango
amewataja watumishi hao kuwa ni pamoja na Harrison Mwampashi, John
Makorere, Stephene Josia na Frank Kessy na kuviagiza vyombo vyote vya
Ulinzi na Usalama mpakani hapo viwahoji huku wakiwa wamesimamishwa kazi.
Watumishi
hao wanadaiwa kuiba lakiri hizo kumi kutoka ofisi za TRA-Tunduma
wanakofanyiakazi, ambapo 4 kati ya hizo lakiri zilikutwa zimefungwa
kwenye mizigo ya malori yanayoshikiliwa katika mpaka huo baada ya
uchunguzi kufanyika huku malori mengine 5 yakizuiwa baada ya kuonekana
lakiri zao zimechezewa.
Taarifa
zinasema kuwa baada ya uchunguzi, mawakala ama wamiliki wa malori hayo
wamedai walipewa lakiri hizo na watuhumiwa na kwamba uchunguzi zaidi
umebaini kuwa kiwango cha mizigo kilichomo kwenye makontena yaliyobeba
mizigo ya magogo na kufungwa lakiri hizo za wizi hakilingani na idadi ya
mizigo iliyoko kwenye nyaraka jambo linaloashiria kuwa wanazitumia
lakiri hizo kudanganya idadi na uzito wa mizigo yao ili kukwepa ushuru
na kodi mbalimbali za Serikali.
“Hakuna
kitu muhimu kama uadilifu kwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato na
hatutasita wala hatutamwonei aibu mtu yeyote, tutachukua hatua kwa
mujibu wa sheria ili kulinda fedha za umma” alionya Dkt. Mpango
Alisema
kuwa Serikali imebaini baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato na
Idara za Forodha mipakani wanashirikiana na wafanyabishara wasio
waaminifu kuingilia mifumo ya kukusanyia mapato, kitendo ambacho
kinaweza kurudisha nyuma juhudi za serikali kuwahudumia wananchi wake.
Dkt.
Mpango amewaonya wafanyakazi wote wa forodha na Mamlaka ya Mapato
nchini, kuwa wazalendo na waaminifu katika kukusanya mapato ya Serikali
na kuacha kujihusisha na vitendo vinavyokwaza ufanisi wa Mamlaka hayo.
BIASHARA YA KUBADILISHA FEDHA MPAKANI
Wakati
huo huo, Dkt. Mpango, ametoa muda wa siku thelathini, kwa
wanaobadilisha fedha za kigeni kiholela mipakani, waache mara moja,
badala yake waheshimu sheria za Nchi, na kuunda vikundi vinavyoweza
kuanzisha maduka ya kubadilisha fedha hizo.
Alitoa
kauli hiyo Mjini Tunduma, wakati akizungumza na wabadilisha fedha
mpakani humo, kwamba serikali itawaheshimu tu wale watakaojiundia
vikundi na kuwa na sehemu wanakoweza kubadilisha fedha kwa kufuata
utaratibu na wala si vinginevyo.
ATEMBELEA UJENZI WA KITUO KIPYA CHA FORODHA NA IDARA YA FORODHA TUNDUMA
Akiwa
Mjini Tunduma, Dkt. Mpango, pamoja na mambo mengine ametembelea na
kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Kituo cha pamoja cha Forodha cha Mpaka
kati ya Tanzania na Zambia Mjini Tunduma.
Pia
ametembela Ofisi ya Idara ya Forodha mpakani hapa, na kupata taarifa ya
makusanyo ya mapato kwa mwaka wa Fedha wa 2016/2017, ambapo maafisa
wamekusanya mapato zaidi ya Bilioni 75 na kuvuka lengo la mapato
waliyokuwa wameyatarajia.
Meneja
wa Idara ya Forodha mikoa ya Mbeya na Songwe, Bw. Jimmy Nsindo amesema
kuwa pamoja na mafanikio hayo, Mpaka huo wa Tanzania na Zambia, ni mpaka
unaoweza kuingilika kirahisi, matokeo yake udhibiti wa mapato unaingia
dosari, huku baadhi ya watanzania wanafanya biashara zinazodaiwa
kuliingizia hasara taifa, zikiwemo za kubadili fedha za kigeni kwa mfumo
usio rasmi.
ASHITUKIZA VITUO VYA MAFUTA
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ametoa muda wa siku ishirini
kwa wamiliki wote wa vituo vya mafuta ambao wameomba kupatiwa mashine
za Kielectroniki kwaajili ya kuunganishwa na mfumo wa kodi na utoaji wa
risti wawe wamepata mashine hizo vinginevyo watafungiwa vituo vyao.
Aidha,
amesema ifikapo Jumatano Juma lijalo wamiliki wote wa maduka mkoani
Mbeya, waanze kutumia mashine za Kielekroniki za kutolea risiti (EFDs)
na kuonya kwamba Serikali haitasita kuyafunga maduka yao wasipotekeleza
maagizo hayo.
Waziri
wa Fedha na Mipango ametumia ziara hii kutoa shukrani kwa wananchi wa
mkoa wa Mbeya namna walivyoitikia kulipa kodi za nyumba.
No comments:
Post a Comment