Na Benny Mwaipaja, WFM, Songwe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Prof. Adolf Mkenda, amewaonya mawakala wa forodha katika mpaka wa
Tanzania na Zambia wa Tunduma/Nakonde kuacha Mara moja tabia ya
kuwachelewesha madereva wa malori yaendayo masafa marefu kwa makusudi
ili wapewe rushwa.
Prof. Mkenda ametoa onyo hilo katika mpaka huo wa Tunduma
na Nakonde, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya madereva
wa malori waliodai wamekuwa wakicheleweshwa kuvuka mpaka huo kwa zaidi
ya siku tatu hadi tano.
Wadereva hao wameeleza kuwa mawakala wa forodha wamekuwa
wakiwaambia kuwa nyaraka zao zinazohusika na mizigo wanayosafirisha
zimekuwa zilicheleshwa na kituo cha Forodha upande wa Zambia.
Hata hivyo Meneja wa Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA),
Kituo cha Nakonde, Bw. Nase Lungu, amekana kuhusika na ucheleweshaji huo
na baada ya ukaguzi wa moja ya nyaraka hizo ilibainika kuwa upande wa
Zambia unatoa nyaraka hizo kwa wakati lakini zimekuwa zikifichwa na
Mawakala wa Forodha upande wa Tanzania.
Wakitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo, madereva hao wamesema
kuwa mawakala wa forodha kwa muda mrefu wamekuwa wakiwaeleza kuwa
mtandao wa intaneti wa Upande wa Zambia unaotumika kuchakata nyaraka zao
uko chini, hivyo walitakiwa kutoa shilingi 10,000 kwa kila nyaraka ili
"kurahisisha" kazi hiyo kwa kuwapa kitu kidogo maafisa wa forodha wa
Zambia.
"Mawakala wengine wa forodha wana nyumba zao za kulala
wageni hapa Tunduma kumbe wanatulazimisha kukaa hapa ili tulale kwenye
nyumba hizo hali inayotutia hasara na wanatumia kutokujua kwetu
kutudanganya kwamba mtandao uko chini wakijua hatuna uwezo wa kufuatilia
huko Zambia" alieleza kwa masikitiko dereva mmoja
Baada ya kubaini uwepo wa vitendo hivyo, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, ameagiza
Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA upande wa Tunduma kuandika kibao chenye
namba za simu za Mkuu wa TRA mpakani hapo zitakazotumiwa na madereva
wanaocheleweshwa kwa makusudi kutoa malalamiko yao.
"Tunataka madereva mtumie siku moja tu kukamilisha
nyaraka zenu ili muendelee na safari yenu vinginevyo tutadumaza biashara
kati ya Zambia na Tanzania na pia tutaifanya Bandari yetu ya Dar es
salaam kushindwa kuleta tija" aliongeza Prof. Mkenda
Alisema kuwa wakala wa forodha atakayebainika kufanya
mchezo huo mchafu wa kuwarubuni madereva na kuwachelewesha kupeleka
mizigo nchini Zambia, watanyang'anywa leseni zao za biashara.
Meneja Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania,
mikoa ya Songwe na Mbeya, Bw. Jomimassa Nsindo, amesema kuwa ofisi yake
itashirikiana na madereva kukomesha vitendo hivyo ambavyo amesema
vinaharibu uchumi na biashara mpakani hapo.
Naye Mkuu wa wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Bw. Juma
Irando, alisema kuwa ataitisha kikao cha Madereva, Mawakala wa Forodha
na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA katika Mpaka huo wa Tunduma/Nakonde
mapema, ili kuweka msimamo wa serikali na kuwaeleza wahusika wanaokiuka
taratibu hatua watakazochukuliwa.
Prof. Mkenda na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, walikwenda katika mpaka huo wa
Tunduma na Nakonde, kuangalia maandalizi ya uanzishwaji wa Kituo cha
Pamoja cha Mpakani kati ya Tanzania na Zambia, unaotarajiwa kuanza
Februari mosi, 2017, baada ya kusainiwa kwa mikataba kati ya nchi hizo
mbili, juzi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment